Tume ya IEBC na wadau wakutana kwenye kongamano KICC

Tume huru ya uchaguzi na mipaka na wadau mbali mbali wa uchaguzi leo wanakutana katika jumba la KICC jijini Nairobi kwa kongamano la kitaifa kuhusu uchaguzi. Kongamano hilo la siku tatu limeandaliwa ili kuweka mikakati itakayotoa mwongozo kwa Wakenya katika kuandaa uchaguzi wa amani. Maswala yatakayojadiliwa kwenye kongamano hilo ni pamoja na mafunzo yaliyotokana na chaguzi zilizopita , uzuiaji na utatuzi wa mizozo, shughuli za uchaguzi na teknolojia na wajibu wa vyombo vya habari miongoni mwa maswala mengine. Kongamano hilo limeandaliwa kwa pamoja na maafisa wa tume ya IEBC , tume ya maadili na kupambana na ufisadi na vugu vugu laA� Kura Yangu, Sauti Yangu ambao watashiriki katika majadiliano kuhusu hali ya kujiandaa kwa Kenya na mkakati mzima wa kulinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu dhidi ya hatari ya kutokea kwa machafuko na uhalifu wa kimtandao. Wengine watakaoshiriki kwenye kongamano hilo ni viongozi wa kisiasa, mashirika ya kijamii , vyombo vya habari na Wakenya kwa jumla.