TSC yamkosoa Sossion kwa kupotosha waalimu

Tume ya kuajiri walimu-TSC imemkosoa katibu mkuu wa chama cha kitaifa cha waalimu KNUT, Wilson Sossion, kwa kuwapotosha waalimu na kujaribu kuhujumu utekelezaji mipango ya mitaala ya masomo. Kwenye taarifa kwa wana-habari, tume hiyo ya TSC ilimlaumu Sossion kwa kuwachochea waalimu ili wasitekeleze majukumu yao, na imetoa onyo kali kwa waalimu ambao watakaidi maagizo ya mwajiri wao.

Tume ya TSC imefafanua kwamba haijatoa ahadi yoyote ya kuwapandisha vyeo waalimu elfu-30, kama anavyodai Sossion. Kadhalika tume hiyo imesema walimu waliohamishwa sharti wafike katika sehemu zao za kazi kwani hatua hiyo inaambatana na majukumu muhimu ya tume ya TSC.

Waalimu wakuu na waalimu pia wameagizwa kutia saini kandarasi za kutathmini utendakazi wa waalimu kwa muhula wa tatu kuambatana na sheria ya tume ya kuwaajiri walimu,  kanuni za utenda kazi kwa waalimu na mkataba wa maelewano kwa kipindi cha mwaka 2017 hadi 2021.