Trump atisha kukatiza msaada kwa nchi inayobatilisha uamuzi wake wa Jerusalem

Rais Donald Trump wa Marekani jana alitishia kukatiza utoaji msaada wa kifedha kwa nchi ambazo zitapiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio la umoja wa mataifa linalohimiza Marekani kubatilisha uamuzi wake wa kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israeli. Balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa, Nikki Haley, kwenye barua kwa majimbo kadhaa ya Marekani jana zilizoangaziwa na shirika la habari la Reuters, alionya kwamba Trump amemtaka kuripoti zile nchi zitakazopiga kura kupinga uamuzi huo wa Marekani. Baraza kuu la umoja wa mataifa litaanda kikao cha dharura leo kufuatia ombi la mataifa ya kiarabu na kiislamu kupigia kura rasimu ya azimio, ambapo Marekani ilipiga kura ya turufu siku ya Jumatatu kwenye mkutano wa baraza la usalama la umoja wa mataifa lenye wanachama 15. Maafisa kadhaa wakuu wa kibalozi walisema onyo la Haley huenda lisibadili jinsi kura itapigwa katika baraza kuu ambako vitisho kama hivyo huwa nadra. Baadhi ya maafisa wa kibalozi walisema onyo kama hizo huenda ni za kuwashawishi tu wapiga kura nchini Marekani. Trump alibatilisha ghafla maongozi ya Marekani ya miongo kadhaa mwezi huu alipotambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israeli na kuzua ghadhabu miongoni mwa Wapalestina na mataifa ya kiarabu.