Trump Apuuzilia Mbali Vitisho Vya Korea Kaskazini

Rais mteule wa marekani Donald Trump amepuuzilia mbali madai ya Korea kaskazini kwamba inatengeneza makombora yanayoweza kushambulia marekani. Kwenye ujumbe katika mtandao wa twitter Trump alipuuzilia mbali madai ya rais Kim Jong-un wa Korea kaskazini kwamba maandalizi yako kwenye hatua ya mwisho akisema kwamba hilo halitatimia. Haijabainika iwapo Trump alikuwa akielezea shaka yake kuhusiana na uwezo wa kinuklia wa Korea kaskazini au alikuwa akipanga hatua za kuzuia hali kama hiyo. Trump pia aliishtumu China kwa kukosa kusaidia kuithibiti nchi hiyo mshirika wake. Alisema kuwa China imekuwa ikijipatia kiasi kikubwa cha pesa na utajiri kutoka kwa marekani kutokana na biashara inayonufaisha upande mmoja lakini haisaidii kuhusiana na swala la Korea kaskazini. Korea kaskazini imetekeleza majaribio mawili ya kinyuklia katika muda wa mwaka mmoja uliopita na kuibua hofu kwamba imepata ufanisi mkubwa katiak utengenezaji silaha za kinuklia. Hata hivyo haijafanikiwa kutekeleza majaribio ya makombora ya masafa marefu. Wataalamu wanakadiria kwamba huenda ikaichukua nchi hiyo muda wa chini ya miaka mitano kuafikia hilo. Rasimu za umoja wa mataifa zimetoa wito kwa nchi hiyo kukomesha majaribio ya kinyuklia na makombora.