Treni Ya Kubeba Mizigo Uganda Yasababisha Kizaazaa

Treni moja ya kubebea mizigo iliyokuwa ikielekea nchini Uganda jana ilipoteza mwelekeo katika eneo la Makupa ilipoondoka kwenye kampuni ya kuhifadhi nafaka na kusababisha zogo huku waporaji wakivamia mabehewa kuiba ngano iliyokuwa ikisafirisha. Polisi waliitwa kuwathibiti waporaji hao walionuia kujinufaisha kutokana na mkasa huo. Mabehewa mawili kati ya 19 yalianguka baharini huku mengine yakikwama kwenye miti. Haikubainishwa mara moja kilichosababisha ajali hiyo lakini maafisa wa shirika la reli nchini waliokuwa kwenye eneo hilo hawangesema lolote kwani hawaruhusiwi kuongea na wanahabari. Hata hivyo baadhi ya wakazi ambao hawakutaka kutambulishwa walidai kwamba hali duni ya barabara ya reli huenda ilisababisha ajali hiyo. Treni ya uokoaji ilipelekwa kwenye eneo hilo kusaidia kuyaondoa mabehewa hayo baharini na kuyarejesha kwenye barabara ya reli.