Tobiko apendekeza uchunguzi dhidi ya mauji ya Pendo na Moraa

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko amependekeza kuanzishwa uchunguzi wa umma kuhusu madai ya mauaji yaliotekelezwa na polisi ya watoto Samantha Pendo na Stephanie Moraa. Hii inafuatia mapendekezo ya halmashauri huru ya kutathmini utendakazi wa polisi-IPOA siku ya Jumatatu ilipowasilisha ripoti kwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma baada ya kukamilisha uchunguzi. Kuhusu kisa cha Moraa, mkurugenzi wa mashtaka ya umma amependekeza kwamba tume ya huduma ya taifa ya polisi inapasa kufidia familia ya marehemu kwa matumizi ya nguvu na polisi kinyume cha sheria. Kadhalika mkurugenzi wa mashtaka ya umma ameshauri familia ya marehemu mtoto Moraa kufungulia mashtaka huduma ya taifa ya polisi ikiwa tume ya huduma hiyo haitawafidia.

Kuhusu kisa cha mtoto Pendo ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma imependekeza tume ya huduma ya taifa ya polisi kuwachukulia hatua za nidhamu makamanda husika wa polisi kwa kutepetea katika utekelezaji kazi yao hasa kwa kushindwa kushirikisha oparesheni husika ya maafisa wa polisi kwenye kisa hicho. Kadhalika Tobiko amewahimiza wazazi wa mtoto Pendo kuifungulia mashtaka huduma ya taifa ya polisi kwa fidia. Polisi walilaumiwa kwa kumgonga kichwani kwa rungu mtoto Pendo aliyekuwa na umri wa miezi sita baada ya kuingia kwa nguvu katika makazi ya wazazi wake katika mtaa wa Nyalenda B, huko Kisumu tarehe 12 mwezi Agosti kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais. Pia walilaumiwa kwa kumuuwa kwa kumpiga risasi, Moraa alipokuwa akicheza A�kwenye roshani ya nyumba yao ya kukodisha katika mtaa wa Mathare North jijini Nairobi tarehe 12 mwezi Agosti.