Tobiko aagiza Uchunguzi wa Ghasia za ODM Migori

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko ameiagiza idara ya upelelezi kuchunguza kiini cha ghasia zilizozuka kwenye mkutano wa chama cha ODM huko Migori hapo jana.Kwenye barua kwa mkurugenzi wa idara ya upelelezi Ndegwa Muhoro, Tobiko ameiagiza idara hiyo kuwasilisha kwa ofisi yake faili ya uchunguzi kuhusu kisa hicho ili waliohusika wafunguliwe mashtaka. Ghasia zilizuka jana wakati wa mkutano wa chama cha ODM katika uwanja wa Posta mjini Migori ,wakati wafwasi wa gavana wa sasa wa kaunti hiyo Okoth Obado walipokabiliana na wale wa mpinzani wake aliyekuwa wakati mmoja waziri wa michezo Ochilo Ayako.Wakati wa ghasia hizo,Salim Manzwana,ambaye ni mlinzi wa gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho,alipigwa risasi mguuni alipokuwa akijaribu kumkinga gavana huyo.Joho alikashifu kisa hicho,ambapo viongozi kadhaa wa walijeruhiwa. Wiki iliyopita kiongozi wa chama hicho Raila Odinga alionya kuwa mwaniaji yeyote atakayezua fujo kuwatisha wapinzani wake,hasa wanawake hatapewa tiketi ya chama hicho.