Tobiko aagiza kuchunguzwa kwa Mudavadi, Orengo na maafisa wa IEBC

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko ameagiza idara ya upelelezi na tume ya kupambana na ufisadi kuchunguza hatia za kiuchaguzi zilizofanywa na maafisa wa tume ya uchaguzi wakati wa uchaguzi mwezi uliopita. Kadhalika Tobiko ameagiza asasi hizo mbili kumchunguza kinara mwenza wa muungano wa NASA Musalia Mudavadi na Seneta wa Siaya James Orengo kwa madai kwamba walichunguza savaa za tume ya IEBC kinyume cha sheria. Kiongozi huyo wa mashtaka ya umma amesema rufaa zimewasilishwa kwake na shirika la kijamii la Kura Yangu Sauti Yangu kuwachunguza maafisa wa tume ya IEBC, ilihali ombi la kutaka maafisa hao wa upinzani kuchunguzwa liliwasilishwa na katibu mkuu wa chama cha Jubilee, Raphael Tuju. Tobiko sasa anataka uchunguzi huo kufanywa katika muda wa siku 21 na faili hiyo kupelekwa kwake kwa ukaguzi kabla ya kutolewa maagizo yafaayo. Nchi hii inatarajiwa kuandaa marudio ya uchaguzi wa Urais tarehe 26 mwezi ujao kama ilivyoagiza mahakama ya juu, ambayo iliamua kwamba uchaguzi mkuu wa tarehe 8 mwezi Agosti ulikumbwa na kasoro na uvunjaji sheria.