Timu ya taifa ya raga yaanzisha matayarisho ya raga duniani

Timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande, Shujaa’ itaanza kampeni yake ya msururu wa pili wa msimu wa mwaka 2017/18 wa raga duniani dhidi ya Ufaransa, jijini Cape Town, Afrika Kusini, kesho.Shujaa imejumwishwa kundini ‘A’ pamoja na mabingwa watetezi duniani Afrika Kusini, Urusi na Ufaransa. Shujaa ilibanduliwa katika kinyang’anyiro cha raundi ya kwanza msimu huu jijini Dubai, iliposhindwa na Australia alama 19 kwa 12 katika nusu fainalini ya timu tano bora,na kumaliza  katika nafasi ya saba. New Zealand iliyomaliza ya pili, imejumwishwa kundini ‘B’ katika mechi za raundi ya ‘Cape Town’ pamoja na Australia, Uhispania na Marekani.Mabingwa watetezi wa raundi ya Cape Town, Uingereza, wako kundini ‘C’, pamoja na Uskoti, Ajentina na Uganda, huku waliokuwa mabingwa wa dunia, Fiji, wakiorodheshwa na mabingwa watetezi wa raundi ya Singapore, Kanada, Samoa na Wales kundini ‘D’. Shujaa itanuia kumaliza miongoni mwa timu kumi bora msimu huu, baada ya matokeo duni msimu jana  lipomaliza ya 12, kwa alama 63.