Timu Ya Roll Ball Ya Kenya Yajianda Kwa Mashindano Ya Afrika Mashariki

Timu ya taifa ya mchezo wa a�?Roll Balla�� inatarajiwa kuanza mazoezi mapema mwezi ujao, kujiandaa kwa mashindano ya Afrika Mashariki yatakayoandaliwa kuanzia tarehe sita hadi nane mwezi Mei, humu nchini.

Baada ya kukamilika kwa mechi za kutafuta mshindi wa ligi kuu humu nchini hapo jana, timu za taifa zitaanza kujiandaa vilivyo huku zikinuia kuonyesha umahiri wao katika mashindano ya Afrika Mashariki. Kocha wa wanaume Jared Onyango amesisitiza kuwa lengo kuu la timu hiyo ni kufanya vyema kwenye mashindano hayo na kujiongezea matumaini ya kupanda katika orodha ya dunia. Timu hiyo kwa sasa inashikilia nafasi ya nne duniani. Aidha, Jacob Nyaudo, anayeifunza timu ya akina dada amefichua kuwa anatarajia timu yake iendelee kutawala katika mchezo huo hasa kwa sasa inapoorodheshwa katika nafasi ya kwanza duniani. Baada ya kikosi cha takriban wachezaji 40 kuchaguliwa jana, timu hizo mbili zitapunguzwa hadi wachezaji 12 katika kila timu.