Thomas Letangule aitaka IEBC kufanyia vifaa vya elektroniki majaribio

Aliyekuwa kamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka- IEBC, Thomas Letangule ameitaka tume hiyo kukagua na kufanyia majaribio vifaa vya elektroniki vitakavyotumiwa katika kupiga kura kuhakikisha viko katika hali nzuri kabla ya kusambazwa kwenye vituo vya kupigia kura. Kwenye mahojiano na shirika la utangazaji la KBC, Letangule alisema tume ya IEBC ina muda wa kutosha kufanyia majaribio vifaa hivyo ili kuhakikisha havikubwi na hitilafu zozote wakati wa uchaguzi mkuu. Alitoa wito kwa Wakenya kuwa na imani na tume ya IEBC na kuunga mkono juhudi za kuandaa uchaguzi mkuu kwa njia ya haki na uwazi. Alieleza matumaini kuwa makamishna wa tume hiyo wamejiandaa vyema kusimamia uchaguzi huo.