Tetemeko la Ardhi Lasababisha Vifo na Ubomoaji Majengo Kusini Mwa Japan

Watu tisa wamefariki na wengine zaidi ya 250 kujeruhiwa baada ya tetemeko kubwa la ardhi kukumba kusini mwa Japan na kubomoa majengo ya kukatiza usambazaji umeme.

Maafisa wamesema watu zaidi huenda wamekwama ndani ya vifusi vya majengo yalioporomoka. Maelfu ya watu walitoroka makazi yao na watu wengi walilala nje huko Mashiki katika mji wa Kumamoto kwenye kisiwa cha Kyushu.

Vikosi vya kijeshi vimepelekwa eneo hilo lakini shughuli za uokoaji zimetatizwa na mitetemeko mingine midogo ya ardhi kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo.

Hakuna onyo la mawimbi ya Tsunami lilitolewa kufuatia tetemeko hilo la ardhi la kiwango cha 6.4A�. Viwanda vya kinuklia katika kisiwa hicho havikuathiriwa na tetemeko hilo.

Viwanda viwili vya kinuklia vya Sendai huko Kyushu vilikuwa vikiendesha shughuli kama kawaida ilhali vile vitatu vya Genkai vilifungwa kwa ukaguzi wa kawaida.