Takribani Watu 20 Wauawa Congo

 

Zaidi ya watu 20 wameuawa kwenye ghasia kati ya waandamanaji na walinda usalama katika mji mkuu wa jamhuri ya demokrasi ya Congo,Kinshasa kuhusiana na hatua ya rais Joseph Kabila kukataa kung’atuka mamlakani.Habari hizo ni kwa mujibu wa duru za Umoja wa mataifa.Kulingana na Jose Maria Aranaz,ambaye ni mkurugenzi wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa mataifa, imethibitishwa kuwa raia 20 wameuawa kwenye ghasia ambazo zimekuwa zikiendelea mjini Kinshasa.Aidha shirika la habari la REUTERS lilisema kuwa hali ya usalama ni mbaya katika mji huo.Liliarifu kuwa baadhi ya waathiriwa walipigwa risasi kwa karibu na walinda usalama.Utawala wa miaka 15 wa rais Kabila ulitarajiwa kumalizika siku ya jumatatu usiku,lakini ameamuru tarehe hiyo kusongezwa mbele hadi mwaka wa 2018.Mpinzani mkuu wa rais Kabila,Moise Katumbi wa chama cha PPRD amesema kuwa hatua ya Kabila kukatalia mamlakani ni kama mapinduzi ya kijeshi.Tume ya uchaguzi ya DR Congo ilifutilia mbali uchaguzi wa urais uliotarajiwa kufanywa mwezi uliopita kutokana na matatizo ya kimipango na kifedha.Rais Kabila amebuni serikali ya mpito ya wanachama 74 kuliongoza taifa hilo hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika nchini humo mwaka wa 2018