Takriban Watu Elf-3 Waliotoroka Vita Warejea Kwao Damasak Nigeria

Zaidi ya watu elf-3 waliotoroka kwao katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria kufuatia harakati za miaka-7 za wanamgambo wa kiislamuA� wamerejea kwao baada ya barabara muhimu kufunguliwa katika eneo hilo. Mji wa Damasak ulioko katika jimbo la Borno ambalo limeathiriwa zaidi na mashambulizi ya wanamgambo ulitekwa na kundi la Boko Haram mwaka-2014. Mji huo ulikombolewa na wanajeshi wa serikali ya Nigeria mwezi julai mwaka huu. Rais Muhammadu Buhari alisema siku ya jumamosi kuwa jeshi lilitwaa kambi muhimu ya wanamgambo wa Boko Haram katika msitu wa Sambisa. Serikali ilisema kuwa barabara mbili muhimu zimefunguliwa tena katika mji wa Maiduguri na kwenye miji ya Damasak na Baga. Zaidi ya watu milioni-2 waliachwa bila makao wakati wa harakati za wanamgambo hao wa Boko Haram wanaotaka kubuni jamhuri huru ya Kiislamu inayozingatia sheria kali za Kiislamu yaani sharia katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria. Zaidi ya watu elf-15 wameuawa kwenye harakati hizo.