Taharuki Yatanda baada ya watu 15 Kuuawa Baringo

Hali ya taharuki imetanda katika kaunti ndogo ya Baringo Kusini baada ya mauaji ya watu-15 jana jioni katika eneo la Mukutani katika kisa cha kulipiza kisasi baina ya jamii za Ilchamus na Wa-Pokot. Mapigano hayo yalizuka pale wanawake wawili kutoka jamii moja walipouawa kwa kupigwa risasi baada ya gari la polisi wa utawala walilokuwa wakisafiria kushambuliwa na majangili karibu na kituo cha Mosuro Center. Baadaye jioni, majambazi kutoka jamii hasimu walitekeleza shambulizi la kulipiza kisasi na kuwaua watu-15. Kwa mujibu wa mwakilishi wa Wodi ya Mukutani, Renson Parkei, wanawake watano na watoto wanne waliuawa kwenye shambulizi hilo la kulipiza kisasi katika shule ya msingi ya Mukutani. Majeruhi wa shambulizi hilo wakiwemo watoto wawili walipelekwa na maafisa wa shirika la msalaba mwekundi katika hospitali ya Marigat ambako walitibiwa. Msichana wa umri wa miaka sita pia alijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali ya St Mary’s Gilgil kaunti ya Nakuru akiwa na risasi kifuani mwake.A� Juhudi za kupata ufafanuzi kutoka kwa afisa mkuu wa polisi wa utawala huko Baringo, Robinson Ndiwa ziligonga mwamba kwani alikuwa kwenye mkutano wa usalama.