Spika Wa Bunge La Kaunti Ya Mombasa Akamatwa Na Maafisa Wa Polisi Katika Maandamano Dhidi Ya IEBC

Spika wa bunge la kaunti ya Mombasa, Thadius Rajwahi na mwakilishi wa wadi ya Junda, Paul Onje wamekamatwa na maafisa wa polisi kufuatia maandamano ya kupinga tume huru ya uchaguzi na mipaka huko pwani. Wawili hao ni miongoni mwa watu wengine waliokamatwa huku maafisa wa polisi wakitawanya waandamanaji wanaotaka makamishna wa IEBC waondoke mamlakani. Waliokamatwa wamezuiwa katika kituo cha polisi cha Central. Walioshuhudia hali hiyo walisema maafisa wa polisi awali walionekana wakishika doria katika barabara za mji huo, ambapo vituo vingi vya biashara vilifungwa kwa kuhofia uharibifu wa mali wakati wa maandamano hayo. Hata hivyo mamia ya waandamanaji walishiriki maandamano hayo yaliyoongozwa na gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho na mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nasir. Wakati uo huo, seneta wa Kakamega, Boni Khalwale amekamatwa alipokuwa akijaribu kuingia katika afisi za IEBC huko Kakamega zilizimwa na maafisa wa polisi. Khalwale ambaye yuko Kakamega kuongoza maandamano dhidi ya tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC, amesema ataendelea na maandamano hayo hadi makamishna wa IEBC watakapoondoka mamlakani akisema maandamano yanaruhusiwa kisheria, huku akimkashifu mbunge wa Starehe, Maina Kamanda ambaye ametishia kuwasilisha kesi mahakamani kupinga maandamano yanayoendelea. Lakini mbunge wa Navakholo, Emmanuel Wangwe amedumisha kwamba sheria sharti izingatiwe katika kuwaondoa makamishna wa IEBC mamlakani.