Situma wa Mathare na Mudavadi wa kakamega homeboyz wapigwa marufuku kushiriki kucheza raundi ya 32 ya KPL

Wachezaji wawili wanaoshiriki katika ligi kuu ya soka humu nchini wamepigwa marufuku na hawatashiriki katika mechi za raundi ya 32 katika timu zao.

James Situma wa Mathare United alioneshwa kadi ya tano ya njano wakati wa mechi dhidi ya Tusker kwa hivyo hatashiriki katika mechi dhidi ya Posta Rangers kesho uwanjani Kasarani jijini Nairobi.  Mchezaji mwengine aliyepigwa marufuku ni wing’a wa timu ya Kakamega Homeboyz, Moses Mudavadi, ambaye pia alioneshwa kaddish ya tano ya njano msimu huu kwa hivyo hatacheza dhidi ya  Sony Sugar kesho nyumbani.

Katika michuano mingine kesho, Kariobangi Sharks itachuana na Wazito iliyo katika hatari ya kushushwa ngazi katika uwanja wa Kaunti ya Machakos huku Nakumatt ikimaliza udhia na Nzoia Sugar uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi.

Bandari itaialika Sofapaka katika uwanja wa Mbaraki jijini Mombasa huku Vihiga United ikigaragazana na mabingwa wa ligi Gor Mahia katika uwanja wa Mumias Complex. Zoo Kericho itaialika Ulinzi Stars huku AFC Leopards ikipimana nguvu na Tusker katika uwanja wa Gatuzi la Machakos.