Sicily Kariuki Atoa Shilingi Milioni 2.25 Kustawisha Wanawake Kibiashara

Waziri wa utumishi wa umma na masuala ya vijana na jinsia Sicily Kariuki, jana alitoa hundi za shilingi milioni 2.25 kutoka hazina ya kustawisha wanawake kibiashara kwa makundi manane ya wanawake katika eneo A�bunge la Mbita, kaunti ya Homa Bay. Akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa michezo wa Mbita ambako alizindua mpango wa shirika la huduma ya vijana kwa taifa-NYS wa kuwapa uwezo vijana katika eneo bunge la Mbita Bi. Kariuki aliwahimiza wanawake kutumia fedha hizo kufadhili miradi ambayo itainua hali yao ya maisha. Alisema ipo haja kwa wanawake kuelemishwa kuhusu usawa wa kijinsia ambao alisema utawapa uwezo wa kuwania nyadhifa za uongozi. Wakati huo huo waziri alitoa wito wa kukomeshwa itikadi duni ambazo zinahujumu haki za wanawake na wasichana. Bi. Kariuki alitaja ukeketaji wasichana na ndoa za mapema kuwa itikadi duni zilizopitwa na wakati ambazo zinazuia ustawi wa mtoto msichana. Waziri Bi. Kariuki aliandamana na mbunge wa eneo hilo Millie Odhiambo. Eneo bunge la Mbita lina vijana 588 wanaoshirika kwenye mpango wa shirika la NYS ambao wana akiba ya shilingi milioni 7.7 katika vyama viwili vya akiba na mikopo.