Sicily Kariuki asema uchunguzi kwenye hospitali ya Kenyatta uharakishwe

Waziri wa Afya, Sicily Kariuki  ametaka uchunguzi  unaofanywa kufuatia kisa ambapo wataalam kwenye hospitali  ya Kitaifa ya  Kenyatta  walifanya upasuaji wa  kichwa  kwa mgonjwa ambaye hakustahili upasuaji huo uharakishwe.  Akiongea baada ya kukutana  na maafisa  wa  Bodi ya Madaktari na wataalam wa Matibabu ya meno Nchini.  Kariuki aliagiza kuwa halmashauri ya hospitali ya  Kitaifa ya Kenyatta  iwasilishe ripoti ya awali  kuhusu swala hilo kwa afisi yake hapo kesho.  Aliitaka  hospitali hiyo kushirikiana kikamilifu  na  Bodi ya Madaktari na wataalam wa Matibabu ya meno ambayo sasa imechukua shughuli ya kuchunguza kisa hicho.  Mwenyekiti wa Bodi ya Madaktari na wataalam wa Matibabu ya meno Profesa  George Magoha amesema bodi hiyo imejitolea  kuhakikisha haki inatekelezwa  kufuatia kisa hicho  lakini akamtaka waziri  kuiagiza hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta kurejesha kazini  daktari  mwanagenzi na  wauguzi wawili  waliokuwa wametimuliwa kufuatia kisa hicho. Bodi hiyo inatarajiwa kukamilisha uchunguzi wake katika muda wa juma moja na kuandaa ripoti itakayowasilishwa kwa waziri wa afya ili achukue hatua zinazofaa.