Shule 30 zinachunguzwa kwa madai ya kunuia kufanya udanganyifu katika mtihani wa KCSE

Serikali  inachunguza shule 30 za sekondari ambako waalimu wakuu na wazazi wanadaiwa kushirikiana ili kufanikisha udanganyifu wa wanafunzi katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha Nne (KCSE).  Akiwahutubia wanahabari katika taasisi ya ustawi wa mitaala, waziri wa elimu Amina Mohammed alionya kuwa serikali itamchukulia hatua kali yeyote atakayepatikana na hatia.

Kadhalika alisema kuwa wasimamizi wa vituo vya mitihani wamepewa maongozi bayana kuhusu utaratibu wa mitihani akiongeza kusema kuwa shughuli hiyo itachunguzwa kupitia kwa simu za rununu kwa saa 24 kwa siku.

Waziri Amina aliyasema haya jana baada ya kuongoza mkutano wa kamati tekelezi kuhusu marekebisho ya mtaala. Taarifa za vyombo vya habari zilisema kuwa baadhi ya walimu wakuu wa shule za sekondari wamekuwa wakikusanya pesa kutoka kwa wazazi ambazo walidai zitasaidia kununua vifaa vya mitihani au kuwalipa wale watakaosimamia mitihani hiyo.