Shughuli za wakimbizi Dadaab zasalia kulemazwa kwa wiki ya upili

Shughuli katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab zimesalia kulemazwa kwa wiki ya pili kufuatia maandamano ya jamii ya eneo hilo dhidi ya shirika la umoja wa mataifa kuhusu wakimbizi UNHCR.Jamii hiyo inashinikiza kubadilishwa kwa msimamizi wa shughuli katika kambi hiyo na msaidizi wake . Shughuli muhimu kama vile usambazaji wa vyakula katika kambi za wakimbizi na huduma za matibabu zimekwamishwa . Baadhi ya viongozi na wazee wa jamii hiyo wameazimia kutoruhusu shughuli yoyote kutekelezwa kwenye kambi hiyo hadi shirika hilo libadilishe msimamizi wa shughuli katika kambi hiyo Jean Bosco na msaidizi wake Ivana Unluova. Wakiongozwa na mwakilishi wa wadi ya Dmajale Diriye Abdi, jamii hiyo wamewatuhumu maafisa hao kwa kufanya maamuzi bila kushauriana na viongozi wa eneo hilo. Jamii hiyo imedai kuwa shirika la UNCHR imetoa ilani ya kusimamisha kazi zaidi ya vijana 100 wa jamii hiyo huku kukiwa na madai kuwa wakimbizi wanaharibu mazingira. Kufuatia maandamano hayo shirika la UNHCR linatarajiwa kukutana na vionozi wa eneo hilo ili kushughulikia hali hiyo.