Shughuli Za Biashara Ya Utalii Lamu Zarejelea Hali Yao Ya Kawaida

Mama wa taifa Margaret Kenyatta amesema shughuli za biashara ya utalii katika kaunti ya Lamu zinarejelea hali zao za kawadia baada ya visa vya ugaidi na ghasia vilivyokumba kaunti hiyo .Bi Kenyata amewapongeza wakazi wa kaunti hiyo wakiongozwa na gavana wao Issa Timamy kutokana na umoja walioonyesha baada ya changamoto za kiusalama zilizokumba kaunti hiyo mwaka 2014 na kujitolea kwao kukuza na kudumisha amani. Amesema utovu wa usalama katika kaunti ya Lamu ulikuwa umewahofisha wawekezaji na watalii. Bi. Kenyatta alikuwa akiongea alipokabidhi kaunti hiyo kliniki maalum ya 40 ya mpango wa Beyond Zero. Kliniki hiyo ilipokewa na gavana Timamy katika uwanja wa shule ya upili ya Mokowe. Mama wa taifa amesema mpango wa Beyond Zero utashirikiana na serikali ya kaunti hiyo kuchangisha pesa za kununua mashua ya ambulansi ili kuhudumia visiwa ambavyo ni sehemu ya kaunti ya Lamu na ambako idadi kubwa ya watu wanaishi. Bi. Kenyatta amepongeza serikali ya kaunti hiyo kwa kuimarisha huduma za afya ikiwemo afya ya kina mama na ukabiliananaji wa ugonjwa wa ukimwi. Aidha amesifu hatua ya kuboresha vitengo vya kujifungulia kina mama katika hospitali za kaunti hiyo .