Shughuli ya kusajili wapiga kura katika magereza kuanza

Shughuli ya kusajili wapiga kura katika mengi ya magereza 118 kote nchini itaanza leo Jumatano tarehe 22 mwezi huu wa Februari. Shughuli hiyo ilikosa kaunza siku ya Jumatatu kama ilivyopangwa isipokuwa katika gereza na Naivasha kutokana na changamoto mbali mbali. Mwenyekiti wa tume ya IEBC Wafula Chebukati amesema kwamba takwimu kutoka kwa idara ya magereza zinaonyesha kwamba kuna jumla ya wafungwa 49,867 humu nchini. Hata hivyo wafungwa hao watahitajika kushiriki katika uchaguzi wa urais pekee. Alisema kwamba shughuli ya kusajili wakenya walioko ugenini ambayo ilianza siku ya Jumatatu itaendelea kwa muda wa siku 14. Shughuli hiyo inaendelea katika balozi za Kenya na pia afisi ndogo za ubalozi nchini Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na pia Afrika kusini. Kuhusu swala la kuhama kwa wapiga kura, Chebukati alisema zaidi ya wakenya milioni moja wamehamisha vituo vyao vya kupigia kura.Chebukati alikariri kwamba tume yake itahakikisha uchaguzi huru na wa haki na akahimiza vyama vyote vya kisiasa na pia wawaniaji wa nyadhifa mbali mbali kuendesha kampeini zao kwa amani na pia kuambatana na sheria.