Shirika La Afya Ulimwenguni WHO Laonya Kuhusu Ongezeko La Ongonjwa Wa Kisukari

Idadi ya watu wazima wanaogua ugonjwa wa kisukari ilifikia milioni 422 mwaka 2014, ongezeko mara nne la idadi ya mwaka 1980 ambayo ilikuwa milioni 108. Haya yamethibitishwa na shirika la afya duiniani-WHO kwenye ripoti yake ya kwanza kuhusu ugonjwa wa kisukari duniani. Haya yamejiri huku Kenya ikiungana na ulimwengu kuadhimisha siku ya afya duniani. Shirika la WHO limetahadharisha kuwa ugonjwa huo umeenea sana kutokana na mabadiliko ya mitindo ya maisha ikiwemo lishe na kazi. Ripoti hiyo inasema ugonjwa huo ulisababisha kwa njia ya moja kwa moja vifo vya watu milioni 1.5 mwaka 2012, lakini watu waliofariki kutokana na athari za ugonjwa huo walikuwa milioni 2.2 mwaka huo huo. Ugonjwa wa kisukari umegawanywa mara mbili na bado hakuna mbinu za kuzuia aina ya kwanza inayotokea wakati mwili unaposhindwa kutoa kemikali ya insulin. Aina ya pili ya ugonjwa huo huhusishwa na kuwa na uzani mkubwa pamoja na mitindo ya maisha miongoni mwa watu wazima na watoto. Ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, juhudi zinapaswa kufanywa ili kuhimiza mabadiliko ya mitindo ya maisha hususan lishe bora na kufanya mazoezi ya viungo vya mwili.o