Shilingi bilioni 46.7 yatengwa kwa ugawi wa bajeti ya ziada

Bunge la taifa jana lilikwenda kwa likizo ya wiki tatu baada ya kupitisha mswada wa ugavi fedha za bajeti ya ziada. Mswada huo unaidhinisha serikali kutumia shilingi bilioni 46.7 zilizopitishwa jana kwenye bajeti ya ziada kufadhili miradi muhimu ya serikali miongoni mwa mradi hiyo marudio ya uchaguzi wa urais tarehe 26 mwezi huu na elimu ya shule ya sekondari bila malipo itakayozinduliwa mwezi Januari mwaka ujao. Bunge la taifa linatarajiwa kurejea vikao vyake wiki moja baada ya uchaguzi. Kwenye bajeti ya ziada shilingi bilioni 12 zilitengewa kufadhili marudio ya uchaguzi wa urais ambapo miongoni mwa mambo mengine shilingi bilioni 2 zitatumiwa kuimarisha vifaa vya mfumo uliotangamanishwa wa usimamizi wa uchaguzi-KIEMS, ununuzi wa vifaa vya uchaguzi, maandalizi, mishahara na marupurupu ya maafisa wa uchaguzi na pia kuwalipa maafisa wa polisi watakaodumisha usalama wakati wa marudio ya uchaguzi wa urais. Kampuni zitakazowasilisha mitandao itakayotumiwa za Safaricom, Airtel na Telkom-Kenya zitatumia shilingi bilioni moja. Wabunge pia walitenga shilingi bilioni 1.5 zaidi kwa hazina ya serikali ya taifa ya ustawi wa maeneo bunge. Wizara ya elimu imekabidhiwa shilingi bilioni 25 za kufadhili elimu ya shule za sekondari bila malipo ikiwa ni pamoja na upanuzi wa muundo misingi ulioko kwa sasa ili kukimu hitaji la wanafunzi wengi zaidi watakajiunga na shule za sekondari..