Sheria mpya za uchaguzi zaanza kutekelezwa

Sheria mpya za uchaguzi zimeanza kutekelezwa baada ya kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali. Sheria hizo zilichapishwa kwenye toleo maalum la gazeti rasmi la serikali lililochapishwa jana. Ilani hiyo ya Oktoba-28, ilichapishwa siku mbili baada ya uchaguzi mpya wa urais. Miongoni mwa vipengele muhimu kwenye sheria hizo ni kwamba itakuwa vigumu kwa mahakama ya juu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais kwa kuzingatia kasoro ama dosari ndogo ndogo. Mwada wa marekebisho ya sheria hizo tata uliwasilishwa kwa rais Uhuru Kenyatta kwa maidhinisho baada ya mabunge yote mawili kuupitisha licha ya upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa wachache katika mabunge yote mawili. Hata hivyo rais mteule alikosa kutia saini mswada huo uwa sheria katika muda wa siku-14 baada ya kupitishwa kufuatia shutuma kwamba zitampendelea yeye. Mnamo Alhamisi taasisi ya Katiba na Kituo cha utawala wazi barani Afrika vilielekea mahakamani kuzuia utekelezwaji wa sheria hizo mpya. Wiki iliyopita mwanaharakati Okiya Omtatah aliishtaki serikali kuhusiana na sheria hizo.