Sherehe zazidi kunoga kwa wanafunzi waliotia fora kwenye mtihani wa KCPE

Sherehe zinazidi kunoga katika shule na nyumbani kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kitaifa wa darasa la nane- KCPE baada ya matokeo kutangazwa hapo jana. Katika kaunti ya Baringo, Lucy Jepkemoi alijinyakulia alama 430 kati ya jumla ya alama 500 . Katika kaunti ya Busia, shule ya Ebenezer iliwaibua wanafunzi bora zaidi katika kaunti hiyo, ambapo Priest Antony na Stanley Barasa walipata alama 434 kila mmoja. Shule hiyo imesema ufanisi huo ulitokana na juhudi na ushirikiano.Huko Ruiru, katika kaunti ya Kiambu, wasichana wameibuka videdea, huku Waithera wa shule ya Tumaini Spire akiongoza kwa alama 431. Mkuu wa shule hiyo Florence Wamaitha alitaja unywaji pombe na utumizi wa dawa za kulevya kuwa sababu za wavulana kutotia fora katika mtihani huo. Katika shule ya Juja preparatory, Bradley Ogola alijinyakulia alama 433, akifuatiwa na Carlton aliyejipatia alama 425 huku Amani Jitutu akipata alama 428. Washikadau katika kaunti ya Kajiado wameipongeza wizara ya elimu kwa kutangaza matokeo ya mtihani huo kwa uadilifu, wakisema kuwa ni jambo ambalo limeipa sura mpya sekta hiyo.