Serikali yatoa sh. bilioni 1.4 kulipa wakulima wa mahindi

Halmashauri ya kitaifa ya nafaka na mazao kuanzia leo itawalipa wakulima wa mahindi waliowasilisha mazao yao kwa maghala ya halmashauri hiyo. Hiyo ni baada ya serikali kutoa shilling billion 1.4 za kuwalipa. Waziri wa fedha Henry Rotich amesema kwamba asilimia 95 ya wakulima waliowasilisha mazao yao wamethibitishwa kuwa halisi kufwatia kukamilika kwa zoezi la kuwasaili.

Rotich alisema haya katika eneo la Kaptagat kaunti ya Uasin Gishu wakati wa mazishi ya meja mstaafu, John Sawe. Mnamo siku ya Ijumaa, waziri wa ugatuzi, Eugene Wamalwa alisema wakulima wadogo 514 kati ya wale 900 ambao wamesailiwa watapewa kipaumbele wakati wa usambazaji wa malipo hayo. Wamalwa alisema wakulima 1,154 walichukua fomu za usaili lakini ni 1,140 waliorejesha fomu hizo. Kuhusiana na ongezeko la ushuru, Rotich aliwahimiza Wakenya kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta maendeleo humu nchini akisema serikali inajizatiti kukabiliana na mfumko wa bei.