Serikali Yatenga Bilioni 1.12 Kuzuia Maduka Ya Jumla Ya Uchumi Kusambaratika

Serikali imeingilia kati kuzuia maduka ya jumla ya Uchumi kusambaratika kwa kutenga shilingi bilioni-1.12. Serikali sasa inasubiri maelezo zaidi kuwasilishwa kwenye baraza la mawaziri na waziri wa ustawi wa viwanda Adan Mohammed kuhusu masharti ya kuwekeza pesa hizo, uwezekano wa maduka hayo kuimarika tena na pia mipango ya ukaguzi wa usimamizi wake.

Wakati huo huo Rais atatilia maanani tashwishi za benki kuu na benki za kibiashara kuhusu mswada wa marekebisho ya benki uliopitishwa hivi punde kabla ya kuamua iwapo atauidhinisha au kuurejesha bungeni. Benki zinapinga kuwekwa kwa viwango vya riba katika alama nne juu ya kiwango cha benki kuu cha asilimia 10.5 zikisema hali hiyo itasababisha kutengwa kwa wachukuaji mikopo.