Serikali Yatakiwa Kufidia Waathiriwa Wa Baada Ya Uchaguzi

Viongozi wa hapa nchini sasa wanaitaka serikali kushughulikia maslahi ya waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 ambao bado hawajalipwa fidia. Wakiongozwa na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, viongozi hao walisema maridhiano ya kweli yataafikiwa pale tu wale walioathiriwa na ghasia hizo watakapopokea fidia kutoka kwa serikali. Viongozi hao walikuwa wakiongea wakati wa mazishi ya Joseph Karuri aliyenusurika wakati kanisa lilipoteketezwa katika eneo la Kiambaa wakati wa ghasia hizo. Karuri mwenye umri wa miakaA�64 alipoteza mkono mmoja wakati ulipokatwa na panga pale alipojaribu kuwakinga wanawake na watoto waliokuwa wametafuta hifadhi ndani ya kanisa hilo ambalo liliteketezwa na kusababisha vifo vya watu 35. Sudi alisema inasikitisha kuona waathiriwa wa ghasia hizo wakiendelea kusononeka kutokana na umaskini uliokithiri, miaka minane baada ya ghasia hizo.