Serikali kugatua huduma za KBC

Serikali inakadiria kugatua huduma za shirika la utangazaji la Kenya KBC kwa minajili ya kuziwezesha serikali za kaunti kuangazia ajenda zao za maendeleo. Katibu katika wizara ya mawasiliano, Samuel Itemere amesema mbali na kuwa na wafanyikazi wenye ujuzi, shirika la KBC pia linasikika kote nchini huku idara ya redio ikiwa na vituo 17 vinavyopeperusha matangazo katika lugha za kiasili. Alisema serikali hizo zinaweza kutumia vituo hivyo kuangazia juhudi za maendeleo. Akiongea kwenye kongamano kuhusu ugatuzi mjini Naivasha, Itemere hata hivyo alisema huenda hatua hiyo ikakumbwa na changamoto kwani serikali za kaunti zitahitajika kugharamia asilimia 40 ya matangazo yake kupitia vituo vya shirika hilo. Itemere alisema serikali ya kitaifa ikishirikiana na mashirika husika kuratibu mikakati itakayohakikisha vyombo vya habari hapa nchini vinatumika kikamilifu kuangazia masuala ya maendeleo magatuzini. Gavana wa kaunti ya Trans-Nzoia, Patrick Khaemba alishutumu vyombo vya habari kwa kudhalalisha ugatuzi kwa kuangazia masuala tata pekee bila kuzingatia mafanikio ya mfumo huo.