Serikali Yajiandaa Kutekeleza Mradi Wa Mfumo Wa Digitali Katika Shule Za Msingi Kote Nchini

Serikali inaimarisha juhudi za kuhakikisha shule zote za msingi kote nchini ziko tayari kuanza kusoma kwa kutumia vifaa vya mfumo wa digitali inapoanza kutekeleza mradi huo. Kundi linalotekeleza mradi huo wiki hii litatoa mafunzo ya kimsingi kwa waalimu wakuu wa shule kuhusu mpango wa mfumo wa kidigitali wa kutoa mafunzo ambao unajulikana kama Digischool kwa maandalizi ya uzinduzi wa mpango huo. Kundi hilo pia litakusanya habari kuhusu maandalizi wa shule ya kutekeleza mfumo wa masomo wa kielektroniki kutoka kwa waalimu wakuu wa shule za msingi kwa lengo la kushirikiana na shule katika kuziandaa kuwa tayari kwa mpango huo. Utathmini wa mradi huo utafanywa wakati wa mkutano wa wajumbe wa kila mwaka wa chama cha waalimu wakuu wa shule za msingi ambao kwa sasa unaendelea huko Mombasa. Mkutano wa mwaka huu una kauli mbiu ya Child Friendly Quality Education. Uzinduzi wa mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano katika sekta ya elimu ni mojawapo ya marekebisho makubwa yanayotekelezwa na serikali.