Serikali Yafafanua Utaratibu Wa Kutoa Vitambulisho Isiolo

Serikali imekanusha madai kuwa shughuli ya kuwasaili wanaotuma maombi ya vitambulisho vya kitaifa katika tarafa ya Isiolo ya kati ina dosari na kwamba inachukua muda mrefu. Kamishna wa kaunti ya Isiolo, George Natembeya amesema shughuli hiyo inachukua muda mfupi kwani maafisa wa usaili lazima wawe makini kuzuia wahamiaji kutoka mataifa jirani ya Somalia na Ethiopia kupata vitambulisho vya Kenya huku wakiwa na nia mbaya. Natembeya aliyekuwa akijibu malalamishi ya baadhi ya vijana kutoka kitongoji cha Bulla Pesa mjini Isiolo alisema muda wa kuwasaili wanaotuma maombi ya vitambulisho hivyo unanuiwa kuhakikisha hakuna mtu atakayepata kitambulisho kwa njia za ulaghai. Alisema usaili wa watu walio na zaidi ya miaka 18 utakuwa wa kina zaidi kwani ni lazima watie saini hati ya kiapo kueleza ni kwa nini wamechelewa kupata stakabadhi hizo. Hapo jana, vijana waliandamana mjini Isiolo wakilalamika kuwa wameshindwa kupata vitambulisho kwani machifu huwa hawapatikani afisini.