Serikali Ya Kaunti Ya Nairobi Kuishtaki Serikali Ya Kitaifa Kutokana Na Malimbikizi Ya Madeni

Serikali ya kaunti ya Nairobi imetishia kuishtaki serikali ya kitaifa kuhusiana na deni la malimbizi ya ada za ardhi la shilingi bilioni62. Ilani iliyochapshwa kwenye magazeti ya humu nchini inaonya kwamba serikali ya kaunti ya Nairobi inadai malipo hayo yakiwemo ada za maegesho. Ilani hiyo ilisema wizara kadhaa hazijalipia ada zao huku wizara ya ulinzi ikidaiwa deni la shilingi milioni-60, taasisi ya utafiti na ustawi wa viwanda, shilingi milioni-67, Huduma ya taifa ya polisi shilingi milioni-65 na afisi ya rais inadaiwa shilingi milioni-63. Tume ya kuajiri maafisa wa bunge inadaiwa shilingi milioni-48, mchapishaji wa serikali shilingi milioni-39 na wizara ya uchukuzi inadaiwa shilingi milioni-34. Serikali ya kitaifa pia haijalipia ada za uegeshaji magari za jumla ya shilingi milioni-390 ambapo afisi ya naibu wa rais inadaiwa shilingi milioni-125, Huduma ya taifa ya polisi shilingi milioni-70, Halmashauri ya ukusanyaji ushuru shilingi milioni-45 na benki kuu ya Kenya shilingi milioni-48.