Serikali Ya Kaunti Ya Kisumu Yazindua Mpango Mpya Wa ICT

Serikali ya kaunti ya Kisumu imezindua mpango wa kidijitali unaolenga kuwapa watu 700 walioachia shule darasa la nane ambao wana umri wa zaidi ya miaka 25 ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano. Akiongea wakati wa uzinduzi wa mpango huo katika makao makuu ya kaunti hiyo , gavana wa kaunti hiyo Jack Ranguma, alisema mpango huo umetokana na ushirikiano miongoni mwa shirika la ACWICT, Wakfu wa Rockefeller, shirika la Microsoft na serikali ya kaunti ya Kisumu. Ranguma amesema mpango huo ni muhimu kwa sababu unanuia kuwekeza katika watu wenye viwango vya chini vya elimu ili kukabiliana na ukosefu wa ajira hapa nchini na kuwapa vijana ujuzi wa kiufundi. Ranguma amesema kaunti hiyo inalenga kuwa na idadi kubwa ya wataalam wa teknolojia. Ranguma amesema mpango huo utakaotekelezwa chini ya mpango wa Transform Kisumu, utaanzishwa katika wadi zote 35 za kaunti hiyo .