Serikali na upinzani wameungana kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Gachagua

Serikali na upinzani wameungana kutoa heshima zao za mwisho kwa gavana wa Nyeri Nderitu Gachagua huku wakiungana na maelfu ya waombolezaji nyumbani kwa marehemu gavana huyo huko Hiriga, eneo bunge la Mathira kaunti ya Nyeri kwa mazishi ya marehemu. Miongoni mwa waombolezaji hao ni Rais Uhuru Kenyatta, Rais wa zamani Mwai Kibaki, kiongozi wa upinzani Raila Odinga na magavana kadhaa miongoni mwa wanasiasa wengine kutoka vyama mbali mbali vya kisiasa. Kaka wa marehemu gavana huyo aliye pia msemaji wa familia, Rigathi Gachagua, awali aliwaambia waombolezaji kwamba ingawa kaka yake alikuwa na wafuasi wengi hakuruhusu watu kuuona mwili wakati wa kusafirishwa kutoka chumba cha kuhifadhia maiti kwa sababu zisizoepukika. Familia imewandalia viti wawakilishi wote 46 wa kaunti ya Nyeri ambao baadhi yao walisema hawatahudhuria mazishi hayo wakitaja hofu ya usalama. Kiongozi wa walio wengine katika bunge la kaunti hiyo Duncan Gituanja alidai kuwa wenzake alipokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu wasiojulikana na wakaonywa dhidi ya kuhudhuria mazishi hayo. Hata hivyo kamanda wa polisi wa eneo hilo Larry Kieng alikanusha madai ya wawakilishi hao wa wadi kuhusu taarifa za vitisho vya kuuawa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii akisema hazina msingi. Gachagua alifariki kutokana na saratani ya kongosho katika hospitali ya Royal Marsden jijini London hapo Februari 24.