Serikali Kununua Mifugo Kutoka Sehemu Kame

Serikali leo itaanzisha mradi wa kununua mifugo katika sehemu zilizoathiriwa na ukame. Kampuni ya utayarishaji nyama ya Kenya Meat Commission inapanga kutumia shilingi milioni-170 kununua mifugo katika kaunti nne za Kwale, Kilifi, Tana River na Lamu katika eneo la Pwani. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Kenya Meat Commission, Joseph Learamo amesema wamefanya maandalizi ya kununua mifugo katika kaunti hizo nne zilizoathiriwa. Alisema kampuni hiyo itashirikiana na serikali za kaunti za Kwale, Kilifi, Tana River na Lamu kutekeleza mradi huo. Wafugaji wamehimizwa kutumia fursa hiyo kuuza mifugo iliyodhoofika kifya. Kampuni ya KMC imesema mifugo hiyo itanunuliwa kwa bei nzuri.