Serikali kufadhili wakulima wa mashamba madogo

Serikali itaanza kusambaza vifaa vya kunyunyizia mashamba maji kwa wakulima wa mashamba madogo hapa nchini katika hatua inayonuiwa kukabiliana na ukame unaoathiri takriban wakenya milioni 3. Waziri wa maji Eugene Wamalwa, alisema hatua hiyo ni sehemu ya agizo la rais Uhuru Kenyatta la kubuni mikakati ya kuepuka ukame na baa la njaa. Akiongea jana wakati wa kusambaza pampu 100 za maji na mabomba ya mita-3,600 kwa makundi ya wakulima wa mashamba madogo katika eneo la Langobaya huko Malindi, katika kaunti ya Kilifi , Wamalwa alisema kaunti za Kilifi na Tana River zina uwezo wa kuitosheleza akiba ya chakula hapa nchini kupitia kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji. Waziri Wamalwa aliyeandamana na mwenzake wa madini, Dan Kazungu, meneja mkuu wa bodi ya kitaifa ya maji, Gitonga Mugambi na mkurugenzi wa bodi ya huduma za maji huko Pwani, Joseph Omwange, alisema hatua hiyo inatimiza ahadi yake ya kuwasaidia wakulima hao alipozuru eneo hilo mwezi disemba mwaka uliopita. Wamalwa alisema serikali itaendelea kuchimba visima ili kuwezesha wakazi kutumia maji hayo kwa mahitaji ya nyumbani na kilimo.