Serikali imeongeza mkopo kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya kadri na vya kiufundi

Waziri wa elimu Dr. Fred Matiangi amesema kwamba serikali imetenga shilingi bilioni- 1.2 badala ya Milioni- 900 hapo awali kwa ajili ya utoaji mikopo kwa wale wanaojiunga na vyuo vya kadri na vile vya mafunzo ya kiufundi humu nchini. Matiangi aliongeza kwamba kila mwanafunzi ambaye hakupata nafasi ya kujiunga na elimu ya vyuo vikuu, ana fursa nyingine ya kufanya hivyo kwa kujiunga na mipango ya mafunzo ya  vyeti na pia diploma. Alikuwa akiongea kwenye hafla ya Wings to fly ambayo ni mradi wa Benki ya Equity wa utoaji misaada kwa wanafunzi wanaohitaji usaidizi wa kujiunga na elimu ya sekondari.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa Benki ya Equity, James Mwangi alitoa wito kwa wakenya kuunga mkono marekebisho yanayotekelezwa katika sekta ya elimu nchini, akisema lengo la marekebisho hayo ni kuwezesha watoto wa humu nchini kukubaliwa popote duniani siku zijazo. Alisema kwamba kati ya wanafunzi 8,144 waliodhaminiwa na mradi huo wa Wings to fly hadi kufanya mtihani ya kidato cha Nne (KCSE) katika muda wa miaka mitano iliyopita, 6,828 kati yao waliweza kujiunga na elimu ya vyuo vikuu.

Kundi la mwaka 2018 la wanafunzi  waliodhaminiwa na mradi wa Wings to fly litafikisha jumla ya wanafunzi 19,260. waliodhaminiwa hadi sasa. Ambapo 12,491 kati yao tayari wamekamilisha mtihani wa kidato cha nne KCSE; huku wanafunzi 5,431 wakijiunga na mpango wa Uanajenzi katika Benki ya Equity.