Sekta Ya Utalii Yatarajiwa Kuimarika Baada Ya Henry Rotich Kutangaza Kutengwa Kwa Ksh. Bilioni 4.5 Kwa Mambo Ya Utalii

Sekta ya Utalii huenda itaimarika baada ya waziri wa fedha Henry Rotich kutangaza shilingi bilioni 4.5 zilizotengwa kutumika kwa shughuli za kutangaza mambo ya utalii. Hata hivyo Waziri wa Utalii Najib Balala aliwahimiza wanasiasa wawe na tahadhari wanapotoa matamshi yao ili kulinda taswira ya nchi hii ambayo ni kituo muhimu cha utalii. Sekta ya utalii imekuwa ikikwamuka taratibu kwa muda wa miaka mitatu iliyopita baada ya kuathiriwa na matukio ya ukosefu wa usalama. Hali hiyo chanya inadhihirishwa na idadi ya watalii wanaotembelea nchi hii ambao wameongezeka kwa asilimia 14 katika muda wa miezi mine ya kwanza ya mwaka huu. Mapema mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza kwamba ada za kiingilio katika mbuga za kitaifa na hifadhi zisitozwe ushuru ziada wa thamani VAT ili kuongeza idadi ya wageni katika mbuga hizo hasa kwa watalii wa ndani mwa nchi, agizo ambalo lilizingatiwa katika bajeti ya mwaka huu. Pato la utalii kwa mwaka huu wa 2016 linatarajiwa kuongezeka baada ya sekta hiyo kuonyesha dalili za ukuaji katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huu wa 2016.