Ruto asema serikali itashirikiana na makanisa ili kuboresha maisha ya wakenya

Naibu Rais William Ruto amesema kuwa serikali itashirikiana na makanisa katika kutekeleza mipango inayolenga kuboresha maisha ya wakenya.

Akiongea wakati wa hafla ya kutawazwa kwa  General Superintendent wa kanisa la  Kenya Assembly of God -KAG askofu  Philip Kitoto  iliyoandaliwa katika eneo la Imara Daima jijini Nairobi, Naibu Rais alisema ili kuafikia ufanisi nchini  juhudi za pamoja zinahitajika kutoka kwa washirika mbali mbali.

Alitoa wito kwa wakenya kuwa katika mstari wa mbele kuchangia katika mahitaji ya Maendeleo nchini.  Ruto alitoa wito kwa mashirika ya kidini kuwa katika mstari wa mbele katika kuunganisha taifa hili kwa kuhimiza urafiki na undugu.

Ruto wakati huo huo alitoa wito kwa viongozi wa makanisa kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa bibilia inatafsiriwa katika lugha zote zilizoko nchini ili kuwawezesha wakenya wote kuilewa kwa urahisi.

Aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka alitoa wito kwa kanisa kutekeleza jukumu muhimu katika kupambana na ufisadi.