Ruto ahakikishia wakenya usalama wao katika marudio ya uchaguzi

Serikali itahakikisha Wakenya wanashiriki kwa njia ya amani kwenye marudio ya uchaguzi wa urais tarehe 17 mwezi Oktoba. Naibu rais William Ruto anasema kwamba ingawaje serikali itatekeleza jukumu lake katika kuhakikisha uchaguzi huo unafanywa kwa njia shwari, Wakenya pia wapasa kutekeleza jukumu lao. Akiongea katika kanisa la Crisco huko Vota kaunti ya Machakos, ambako alihudhuria ibada ya Jumapili, naibu rais aliwahimiza Wakristo kuwaombea viongozi kushiriki kwenye kampeni za amani na pia tume ya uchaguzi IEBC ili itekeleze vyema jukumu lake la kusimamia uchaguzi. Naibu rais pia aliwahakikishia Wakenya kwamba watahiniwa milioni 1.5 wa kidato cha nne na darasa la nane watafanya mitihani yao kama ilivyopangwa. Aliwataka viongozi kujali maslahi ya wanafunzi na wasivuruge ratiba ya mitihani.