Rotich awasilisha bajeti ya trilioni 3 huku akikiri kuongezeka kwa deni la kitaifa

Bajeti ya mwaka huu ni ya jumla ya shilingi trilioni 3.074 ambayo ni nyongeza ya asilimia 10.83 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana ya jumla ya shilingi trilioni 2.77. Akiwasilisha makadirio yaliyoko kwenye bajeti ya mwaka huu bungeni yenye kauli mbiu ya “Kubuni nafasi za ajira na kubadilisha maisha” waziri wa fedha Henry Rotich alisema bajeti ya mwaka huu inatoa fursa ya kukabiliana na changamoto zinazokumba nchi hii katika kubuni nafasi za ajira kwa vijana na kuwanufaisha Wakenya wote. Huku akikiri kuongezeka kwa deni la kitaifa waziri wa fedha alisema kipaumbele kimetolewa kwa sekta ya utengenezaji bidhaa, kujitosheleza kwa chakula na kupatikana kwa nyumba za gharama nafuu huku serikali ikilenga kubuni nafasi laki nane za ajira.

Ikizingatiwa kuimarika mazingira ya kisiasa, waziri Rotich amesema wizara yake ina mipango ya kuimarisha ukuaji uchumi kupitia kiwango cha sasa cha asilimia 5.6 huku ikihakikisha deni lake linaweza kulipwa. Aliongeza kusema kwamba uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.8 mwaka huu kutokana na imani ya wawekezaji, kuimarishwa uzalishaji katika sekta ya kilimo kutokana na hali nzuri ya hewa, uwekezaji katika sekta ya umma na kuimarika uuzaji bidhaa. Miongoni mwa sekta zinazotarajiwa kuimarisha ukuaji uchumi ni pamoja na sekta ya utalii ambayo inaendelea kuimarika kutokana na kuimarika kwa hali ya usalama hapa nchini pamoja na kupunguza matumizi serikalini na ufadhili wa ajenda nne kuu za maendeleo.

Waziri Rotich ametaja kukamilishwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa kuwa hatua muhimu akisema Wakenya wengi sasa wanafurahia usafiri wa haraka kwa gharama nafuu kati ya Nairobi na Mombasa. Kadhalika alisema usalama umeimarishwa kote nchini kupitia uwekezaji katika huduma ya taifa ya polisi na kuboresha vikosi vya ulinzi. Wakati huo huo Rotich amesema serikali imeimarisha sekta ya elimu ili kukuza  talanta zinazohitajika hapa nchini kwa kupanua mpango wa elimu bila malipo kwa kujumuisha elimu ya kutwa bila malipo katika shule za sekondari. Kuhusu kuongezeka kwa biashara haramu, waziri amesema kundi la taasisi mbali mbali linajizatiti kutambua na kuharibu bidhaa duni zinazoingizwa hapa nchini ili kukabiliana na biashara haramu ambazo zinaipokonya nchi hii mabilioni ya pesa za mapato.