Riek Machar Atoa Hakikisho La Kurejea Jijini Juba

Kiongozi wa waasi nchini Sudan kusini Riek Machar ametoa hakikisho kwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon kwa njia ya simu kuwa atarejea jijini Juba mwezi ujao wa machi ili kutwaa wadhifa wa makamu wa rais wa kwanza nchini humo. Machar alisema kuwa alikuwa anasubiri kutekelezwa kwa awamu ya kwanza ya mipango ya usalama kama ilivyoafikiwa katika mkataba wa amani. Machar alisema kuwa mkataba huo ulikuwa ukikosa rasilmali zifaazo za kufanikisha utekelezaji wake swala ambalo alisema kuwa aligusia katika mkutano wa hivi maajuzi na viongozi wa mataifa ya Afrika. Machar aliahidi kuunga mkono utekelezaji kamili wa mkataba huo ambao alitia saini kwa pamoja na rais Salva Kiir. Matamshi yake yanawadia baada ya katibu huyo mkuu wa umoja wa mataifa kukutana na Salvar kiir hapo jana. Ban Ki-Moon alitaka kujua iwapo Machar atakuwa jijini Juba kuapishwa na kuwezesha kubuniwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa lengo la kurejesha amani katika taifa hilo changa zaidi ulimwenguni.