Rex Tillerson atarajiwa nchini

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani, Rex Tillerson anatarajiwa humu nchini leo alasiri. Tillerson ambaye alianza ziara yake ya kwanza barani Afrika hapo jana kwa kuzuru Ethiopia, atakutana na rais Uhuru Kenyatta na maafisa wengine wakuu wa serikali kwa mashauriano yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Kenya na Marekani. Tillerson atazuru Chad, Djibouti, Ethiopia na Nigeria. Miongoni mwa maswala yatakayoangaziwa ni vita dhidi ya ugaidi, harakati za kudumisha amani, uongozi bora, ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji. Hapo jana, Tillerson alikutana na kiongozi wa jumuia ya Afrika, Faki Mahamat ambaye alisema bara la Afrika limesahau matamshi ya kukejeli yaliotolewa na rais Donald Trump. Tillerson na Mahamat walijadili maswala ya usalama, tatizo la ugaidi, biashara na maendeleo, ufisadi na mizozo barani humo walipokutana kwenye makao makuu ya Jumuia ya Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia