Rex Tilerson aondoka nchini

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani Rex Tilerson ameondoka humu nchini baada ya ziara ya siku tatu ambapo alikutana na rais Kenyatta na maafisa wengine serikalini. Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Monica Juma, balozi wa Marekani hapa nchini Robert Godec na maafisa wengine wa serikali waliandamana na Tilerson hadi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta. Tilerson alizuru Djibouti na Ethiopia kabla ya kufanya ziara humu nchini na sasa anaelekea nchini Chad. Jana Tillerson alifanya mashauri jijini Nairobi na Bi. Juma na mwenzake wa utalii Najib Balala. Taarifa kutoka wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ilisema mkutano huo ulijadili mikakati ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hii na Marekani. Juma na Tilerson walikubaliana kufanya mashauri ya kila baada ya miaka miwili kuhusu uhusiano kati ya nchi hizi mbili na kujadili na kutia saini makubaliano kuhusu biashara na uwekezaji. Mashauri hayo yalifuatia yale ya siku ya Ijumaa kati ya Tillerson na rais Uhuru Kenyatta.