Real Madrid kunoa makali yake dhidi ya vigogo Atletico Madrid leo usiku

Real Madrid na Atletico Madrid zitafufua uhasimu wao katika mechi ya nusu fainali ya ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya leo usiku.

Real, almaarufu Los Blancos, iliwashinda wenzao katika fainali za mwaka 2014 na 2016, na katika robo fainali ya mwaka 2015. Tangu mwaka 2014, Madrid imeishinda Atletico mara mbili pekee katika michuano 13, huku Atletico ikishinda mara tano na kutoka sare mara sita. Madrid, inayofunzwa na Zinedine Zidane ilihitaji bao la mlinzi Marcelo katika dakika za mwisho mwisho kuishinda Valencia na kujiongezea matumaini ya kutwaa taji ya ligi kuu nchini Uhispania. Atletico, ianyofunzwa na Diego Simeone, itakosa huduma za walinzi Jose Gimenez na Juanfran Torres, na huenda wasirejee katika mechi ya mkondo wa pili uwanjani Vicente Calderon juma lijalo. Mkufunzi wa Madrid, Zidane, ameonya kuwa Atletico huenda ikajipa motisha baada ya kupoteza mechi za hapo awali dhidi ya Madrid.