Rais Wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Awasili Nchini Kwa Ziara Ya Siku Tatu

Rais Uhuru Kenyatta leo asubuhi alimpokea rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika ikulu ya Nairobi ambako alitunukiwa heshima ya mizinga 21. Erdogan ambaye yuko katika ziara ya siku tatu hapa nchini aliwasili katika ikulu ya Nairobi mwendo saa tano asubuhi akiandamana na mkewe Emine Erdogan. Kisha rais huyo wa Uturuki alikagua gwaride la heshima kabla ya kushauriana na rais Kenyatta. Leo alasiri, rais Kenyatta na rais Erdogan watahudhuria mkutano wa kibiashara kati ya wajumbe wa mataifa hayo mawili katika hoteli ya Villa Rosa Kempinski. Awali, rais Erdogan aliweka shada la maua kwenye kaburi la mwanzilishi wa taifa hili hayati Mzee Jomo Kenyatta katika majengo ya bunge. Alilakiwa na spika wa bunge la taifa Justin Muturi na mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Kenya, jenerali Samson Mwathethe.