Rais Uhuru Kenyatta Amkaribisha Waziri Mkuu Wa Israel, Benjamin Netanyahu Katika Ikulu

Rais Uhuru Kenyatta leo asubuhi alimkaribisha waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu katika ikulu ya Nairobi kwenye hafla ya kufana iliyohusisha ufyatuaji mizinga 21. Netanyahu ambaye yuko kwa ziara ya siku tatu hapa nchini alianza ziara hiyo kwa kuweka shada la maua kwenye kaburi la rais wa kwanza wa taifa hili hayati Mzee Jomo Kenyatta. Baadaye Netanyahu akiandamana na mkewe, Sara walitembelea ikulu ya Nairobi ambako alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na kikosi cha jeshi la wanahewa. Kwenye ikulu, Netanyahu alilakiwa na watu mashuhuri akiwemo mama wa taifa,A�Margaret Kenyatta, mawaziri kadhaa na mkuu wa majeshi ya Kenya Jenerali Samson Mwathethe. Baadaye alitia sahihi kitabu cha wageni kabla ya kufanya majadiliano ya moja kwa moja na rais Uhuru Kenyatta. Baadaye leo viongozi hao wawili watahutubia mkutano wa pamoja wa wafanyibiashara kutoka mataifa hayo. Hii ni ziara ya kwanza ya waziri mkuu wa Israeli hapa nchini.