Rais Uhuru Kenyatta Alirejea Nchini Jana Baada Ya Ziara Ya Siku Tatu Botswana

Rais Uhuru Kenyatta alirejea nchini jana baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu ya kiserikali huko Botswana ambako alishinikiza kuchunguzwa upya kwa sheria zinazozuia nafasi za biashara na ajira kati ya nchi hizi mbili. Rais ambaye aliwasili nchini Botswana siku ya Jumatatu asubuhi kwanza alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Ian Khama, kujadili maswala yanayohusu nchi hizi mbili. Akiwa nchini Botswana ajenda kuu wakati wa mazungumzo hayo ilikuwa kuchunguzwa upya kwa sheria za uhamiaji zinazofanya kupata vibali vya kufanya kazi kuwa na masharti magumu. Rais Khama alikubali kuchunguza upya sharia hizo ili Wakenya waweze kuendelea kupata ajira na nafasi za kazi katika nchi hiyo. Pia viongozi hao wawili waliafikia mkataba wa kutathmini mkataba wa huduma za anga unaosimamia masafa ya safari za ndege na vituo vya ndege za shirika la ndege la Kenya huko Botswana. Marais hao wawili pia walishuhudia kutiwa saini kwa mikataba kati ya nchi hizi mbili katika nyanja za uchimbaji madini na huduma za maji. Wakati wa ziara hiyo Rais Kenyatta alifungua semina ya kibiashara kati ya Botswana na Kenya iliyowaleta pamoja wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili kutafuta njia za ushirikiano. Rais atakuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wakati wa ziara yake ya siku tatu humu nchini kuanzia Julai 4 mwaka huu.